• 7:22 AM
  • Mbeya Info

kilimo cha ufuta

KILIMO BORA CHA UFUTA
Ufuta (sesamum indicum)ni zao linalolimwa kwa
wingi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani,
Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika
mikoa ya Rukwa na Mbeya. Zao hili hulimwa kwa ajili
ya chakula na biashara. Mbegu za zao hili huwa na
wastani wa mafuta kiasi cha asilimia 45.
MAMBO YA KUZINGATIA WA KATI WA KUZALISHA
MBEGU
• Chagua aina ya mbegu inayotoa mazao mengi na
bora, inayovumilia mashambulizi ya magonjwa na
wadudu, inayokomaa mapema na kutoa mafuta
mengi.
• Chagua mbegu inayokomaa kwa pamoja ili
kurahisisha uvunaji na pia kuepuka upotevu wa zao
shambani.
• Aina nyeupe ya mbegu ya ufuta hupendelewa zaidi
kuliko aina nyeusi.
MBOLEA
Ufuta unahitaji rutuba ya kutosha ili kutoa mazao
bora. Katika kudumisha rutuba ya udongo, tumia
kilimo cha mzunguko wa mazao au weka mbolea za
asili pale inapobidi.
PALIZI
Dhibiti magugu kwa kupalilia ili kuruhusu ufuta
kutumia vizuri unyevu na virutubishi. Magugu mengine
huwa ni maficho ya wadudu waharibifu wa zao la
ufuta.
MAGONJWA NA WADUDU
Ufuta hushambuliwa na magonjwa na wadudu
mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na
ubora wa mazao. Hivyo kagua shamba mara kwa
mara hasa kwenye maua na mapodo ili kuona dalili za
mashambulizi. Endapo kuna dalili zamashambulizi,
chukua tahadhari mapema kabla ya uharibifu mkubwa
haujatokea.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNAKAGUA SHAMBA
• Kagua shamba kuona kama ufuta umekomaa.
• Ufuta hukomaa, kati ya miezi mitatu na minne tangu
kupanda kutegemea aina.
• Aina ya ufuta usiokuwa na matawi hukomaa
mapema kuliko ile yenye matawi.
• Ni muhimu kuwahi kuvuna ili kuepuka ufuta
kupukutikia shambani.
DALILI ZA KUKOMAA UFUTA SHAMBANI
• Kwa kawaida majani hubadilika rangi kutoka kijani
na kuwa ya manjano na hatimaye kudondoka.
• Mashina hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya
kahawia.
VIFAA VYA KUVUNIA
• Kamba
• Siko
• Panga
VIFAA VYA KUKAUSHIA
• Sehemu ya kukaushia yenye Sakafu ya saruji
• Maturubai
• Sakafu safi
USAFIRI
• Mikokoteni
• Matela ya matrekta
• Magari
KUVUNA
• Vuna ufuta mapema kabla mapodo kukomaa sana
na kuanza kupasuka na kuachia punje.Mapodo ya
ufuta yaliyokomaa sana yakiguswa au kutikiswa na
upepo hupasuka na kuachia mbegu, hali
inayosababisha upotevu mkubwa.
• Mbegu za ufuta ni ndogo na zikidondoka chini ni
vigumu kuziokota. Vilevile mbegu zilizodondoka ni
vigumu kuzitenganisha na uchafu.
• Uvunaji wa ufuta huhusisha ukataji wa mimea yenye
mapodo kwa kutumia vyombo vya mkono kama panga
kwa kukata mashina.
• Kwa aina za ufuta zenye mapodo yanayopasuka,
uvunaji ufanyike wakati mimea bado ni kijani ili
kuepuka upotevu wa mbegu.
• Aidha uvunaji ufanyike wakati hakuna upepo wala
jua kali.
• Baada ya kukata mashina yafunge katika mizigo
midogo na kuweka katika vyombo vya kusafirisha
kama vile mikokoteni, matela au magari hadi sehemu
ya kukaushia.
• Panga mizigo midogo kwa kusimamisha katika
malundo madogo yasiyozidi mizigo minane kwenye
sehemu safi za kukaushia.
KUKAUSHA
Mapodo ya ufuta hukaushwa yakiwa yamefungwa
katika vitita. Vitita huwekwa kwa kuegeshwa kwenye
fremu ya kukaushia kwa muda wa wiki mbili hadi tatu
kutegemea hali ya hewa. Fremu hii huwekwa juu ya
turubai au sakafu ili kuzuia upotevu wa punje
kutokana na kupasuka kwa mapodo.
KUPURA
Upuraji hufanyika kwenye turubai, mkeka au kwenye
sakafu safi.
• Vitita hupigwa taratibu kwa kutumia mti au
hutikiswa vikiwa vimegeuzwa vichwa chini ili
kuruhusu punje za ufuta kudondoka kwenye sakafu
safi au turubai.
KUPEPETA NA KUPEMBUA
Kupepeta na kupembua hufanywa ili kuondoa
takataka kama vile mawe, vipande vya mapodo,vijiti
na vumbi.Njia bora ya kupepeta na kupembua ni kwa
kutumia mikono.
• Ufuta huwekwa kwenye vyombo kama vile ungo kwa
kiasi cha kilo mbili hadi tatu. Ufuta hurushwa hewani
kwa kasi ndogo na takataka nyepesi huchukuliwa na
upepo. Zile nzito huondolewa kwa mikono.
KUFUNGASHA
Mbegu za ufuta zilizo safi huwekwa kwenye
vifungashio kama vile magunia madogo ya aina ya
juti ya ujazo wa kilo 50.
• Fungasha mbegu za ufuta kwenye magunia yenye
uzito usiozidi kilo 50. Kabla ya kufungasha hakikisha
mbegu zimekauka hadi kufikia unyevu wa asilimia 10.
KUHIFADHI
• Panga magunia ya ufuta juu ya chaga.
• Panga kwa kupishanisha ili kuruhusu mzunguko wa
hewa kati ya magunia.
KUSINDIKA MBEGU ZA UFUTA
Ufuta husindikwa kupata bidhaa ya mafuta ambayo
hutumika katika mapishi mbalimbali. Mafuta
hukamuliwa kwa kutumia njia za asili na kwa kutumia
mashine. Njia za asili zina ufanisi mdogo
ukilinganisha na zile za kukamua kwa mashine, hivyo
ni vyema kutumia mashine. Kuna mashine za aina
mbili zinazotumika kukamua mafuta; mashine za
mkono na zile zinazoendeshwa kwa injini au mota ya
umeme. Mashine za mikono zinazotumika zaidi hapa
nchini ni za aina ya daraja (Bridge press) na Ram.
KUKAMUA KWA MASHINE YA DARAJA
Mashine ya daraja ni moja ya mashine za kisasa
zinazoweza kukamua mafuta ya ufuta. Mashine hizi
huendeshwa kwa mikono na zina uwezo wa kukamua
mafuta kwa asilimia 68 hadi 72. Inaweza kukamua
kilo 25 za ufuta kwa saa moja. Ili kupata ufanisi
mzuri wa mashine hii, ni muhimu ufuta uwe na
unyevu wa kati ya asilimia 11 na 13. Iwapo unyevu
utakuwa chini ya kiwango hicho inashauriwa
kunyunyizi maji kwenye ufuta kabla ya kukamua.
VIFAA VYA KUKAMULIA MAFUTA
• Mashine ya daraja
• Sufuria • Vifungashio
• Mifuko midogo ya nguo au viroba vyenye upana wa
sentimita 20 na urefu wa sentimita 20.
• Chombo cha kukinga mafuta.
• Chujio safi
• Lebo
• Lakiri Malighafi
• Mbegu za ufuta safi
• Maji safi
UKAMUAJI MAFUTA
• Nyunyuzia maji kidogo kwenye ufuta ili kuongeza
unyevu kufikia asilimia 11 hadi 13. Mafuta hutoka
vizuri kwenye kiwango hicho cha unyevu.
• Jaza ufuta kwenye vifuko vya nguo au viroba
• Vipange vifuko hivyo kwenye silinda na kuanza
kuzungusha mhimili hadi mafuta yaanze kutoka
kupitia matundu ya silinda.
• Acha kwa muda mafuta yaendelee kutoka kisha
endelea kuzungusha mhimili hadi mafuta yaishe.
Mhimili ukiacha kuzunguka ni dalili kuwa mafuta
yamekwisha.
• Kusanya mafuta, chuja na fungasha kwenye chupa
safi zilizochemshwa. Hakikisha chupa ni kavu na zina
mifuniko.
• Weka lebo na lakiri
• Hifadhi mahali pakavu na pasipo na mwanga mkali.
MASHINE YA RAM
Mashine ya Ram ina uwezo wa kusindika kilo 7 za
mbegu za ufuta kwa ufanisi wa asilimia 57%.Aina ya
Ram (BP-30) ina uwezo wa kukamua lita 20 za
mafuta kwa siku.
VIFAA
• Ndoo
• Mashine ya Ram
• Kichujio au kitmbaa safi
• Vifungashio safi
UKAMUAJI
• Anika mbegu za ufuta juani kwa kuzitandaza
kwenye mabati ili zipate joto la kutosha.
• Lengo la kuanika mbegu juani ni kurahisisha
ukamuaji wa mafuta.
• Jaza mbegu za ufuta kwenye mpare wa kulishia
• Funga wenzozuia (HANDLE)ili mbegu za ufuta
zisitoke.
• Nyanyua wenzozuia mpaka juu ili kuruhusu mbegu
za ufuta kuingia kwenye silinda.
• Shusha wenzozuia chini ili kuruhusu pistoni
kusukuma mbegu za ufuta ziingie ndani ya eneo la
shindilio
. • Nyanyua tena wenzozuia mpaka juu na kushusha
na wakati huohuo ukiendelea kujaza mbegu za ufuta
kwenye mpare wa kulishia. Wenzoinua ukiwa mzito ni
dalili kuwa msukumo wa kutosha umejengeka.
Msukumo huo utasababisha mafuta kutoka.
• Mafuta yanapoanza kutoka legeza wenzozuia ili
kuruhusu mashudu kutoka.
• Chuja na hifadhi mafuta kwenye vyombo safi vyenye
mifuniko vilivyochemshwa.
MATUMIZI
Mafuta ya ufuta hutumika katika mapishi mbalimbali
ili kuongeza ladha. Pia husaidia kuleta nguvu na joto
mwilini. Mbegu za ufuta huchanganywa na vyakula
mbali mbali kama mikate, keki, mboga na kadhalika.
Kwa hisani ya mdau MITIKI -KILIMO KWANZA:
KILIMO BORA CHA UFUTA
By frankclemence:
UFUTA
Ni zao linalostahimili baridi na hulimwa maeneo
yasiyozidi mita 1500 juu ya usawa wa bahari.Mvua ni
Kati ya milimita 400-500 ambazo hutosha kabisa kutoa
mavuno Mengi.
AINA ZA MBEGU
Ziada 94,inakomaa Kwa siku 120-130 na inastahimili
magonjwa.Ina uwezo wa kutoa mavuno zaidi ya kilo
1000 Kwa heka.
Nal 92,inakomaa Kwa siku 90-110 na inastahimili
magonjwa hasa mabaka ya majani.Ina uwezo wa kutoa
mavuno kiasi cha kilo 1200-1500 Kwa heka.
MAGONJWA NA NAMNA YA KUYAZUIA
Magonjwa makubwa ya UFUTA ni mabaka na ukungu
kwenye majani.Magonjwa haya yasipozuiwa
yatapukutisha majani na hivyo kusababisha Mazao
kupungua.
KIZUIA
Panda UFUTA mapema
Tumia mboga zinazostahimili magonjwa Kama-Nal
92
Ng'o mimea iliyoathirika
Tumia kilimo cha mzunguko
Email ThisBlogThis!Share to XShare to Facebook
← Newer Post Older Post → Home

Copyright © Mjasiriamali | Powered by Blogger